Isaiah 24

Dunia Kuharibiwa Upesi


1 aTazama, Bwana ataifanya dunia kuwa ukiwa
na kuiharibu,
naye atauharibu uso wake
na kutawanya wakaao ndani yake:

2 bndivyo itakavyokuwa
kwa makuhani na kwa watu,
kwa bwana na kwa mtumishi,
kwa bibi na kwa mtumishi wake wa kike,
kwa muuzaji na kwa mnunuzi,
kwa mkopaji na kwa mkopeshaji,
kwa mdaiwa na kwa mdai.

3 cDunia itaharibiwa kabisa
na kutekwa nyara kabisa.
Bwana amesema neno hili.


4 dDunia inakauka na kunyauka,
dunia inanyong’onyea na kunyauka,
waliotukuzwa wa dunia wananyong’onyea.

5 eDunia imetiwa unajisi na watu wake;
wameacha kutii sheria,
wamevunja amri
na kuvunja agano la milele.

6 f gKwa hiyo laana inaiteketeza dunia,
watu wake lazima waichukue hatia yao.
Kwa hiyo wakazi wa dunia wameteketezwa,
nao waliosalia ni wachache sana.

7 hDivai mpya inakauka na mzabibu unanyauka,
watu wote wafurahishao wanalia kwa huzuni.

8 iFuraha ya matoazi imekoma,
kelele za wenye furaha zimekoma,
shangwe za kinubi zimenyamaza.

9 jHawanywi tena mvinyo pamoja na wimbo,
kileo ni kichungu kwa wanywaji wake.

10 kMji ulioharibiwa umekuwa ukiwa,
mlango wa kila nyumba umefungwa.

11 lBarabarani wanalilia kupata mvinyo,
furaha yote imegeuka kuwa majonzi,
furaha yote imefukuziwa mbali na dunia.

12 mMji umeachwa katika uharibifu,
lango lake limevunjwa vipande.

13 nNdivyo itakavyokuwa duniani
na miongoni mwa mataifa,
kama vile wakati mzeituni upigwavyo,
au kama vile wakati masazo yabakiavyo baada ya zabibu kuvunwa.


14 oWanainua sauti zao, wanapiga kelele kwa furaha,
kutoka magharibi wanasifu kwa ukelele utukufu wa Bwana.

15 pKwa hiyo upande wa mashariki mpeni Bwana utukufu,
liadhimisheni jina la Bwana, Mungu wa Israeli,
katika visiwa vya bahari.

16 qKutoka miisho ya dunia tunasikia uimbaji:
“Utukufu kwa Yule Mwenye Haki.”

Lakini nilisema, “Ninadhoofika, ninadhoofika!
Ole wangu!
Watenda hila wanasaliti!
Kwa hila watenda hila wanasaliti!”

17 rHofu, shimo na mtego vinakungojea,
ewe mtu ukaaye duniani.

18 sKila akimbiaye asikiapo sauti ya hofu
atatumbukia shimoni,
naye yeyote apandaye kutoka shimoni,
atanaswa kwenye mtego.

Malango ya gharika ya mbinguni yamefunguliwa,
misingi ya dunia inatikisika.

19 tDunia imepasuka,
dunia imechanika,
dunia imetikiswa kabisa.

20 uDunia inapepesuka kama mlevi,
inayumbayumba kama kibanda kwenye upepo;
imelemewa sana na mzigo wa hatia ya uasi wake
na ikianguka kamwe haitainuka tena.


21 vKatika siku ile Bwana ataadhibu
nguvu zilizoko mbinguni juu,
na wafalme walioko duniani chini.

22 wWatakusanywa pamoja
kama wafungwa waliofungwa gerezani,
watafungiwa gerezani
na kuadhibiwa baada ya siku nyingi.

23 xMwezi utatiwa haya, nalo jua litaaibishwa;
kwa maana Bwana Mwenye Nguvu Zote atawala
juu ya Mlima Sayuni na katika Yerusalemu,
tena mbele ya wazee wake kwa utukufu.
Copyright information for SwhKC